Askari Polisi ‘amkaanga’ Sheikh Ponda mahakamani


Mpelelezi wa Jeshi la Polisi, Stesheni Sajenti Juma, ameiambia mahakama kuwa alielezwa na Sheikh Ponda Issa Ponda, kuwa yeye (Sheikh Ponda) ni mhusika katika watu waliojenga msikiti wa muda kwenye kiwanja cha Markaz Chang’ombe kinachodaiwa kuvamiwa na watuhumiwa wenzake.  Juma (52), ambaye ni wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, jana.

Alidai Sheikh Ponda alieleza hivyo wakati akimhoji mbele ya wakili wake katika Kituo cha Kati cha Polisi, Oktoba 17, mwaka jana.
Juma alidai katika maelezo yake, Sheikh Ponda alidai kiwanja hicho ni cha Waislamu na kwamba, mtu anayedaiwa kukimiliki hawamtambui.
Hata hivyo, Juma alidai katika upelelezi alioufanya, alibaini mmiliki halali wa eneo hilo ni Hafidh na kwamba, alithibitishiwa hilo na Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata). Alidai kwa mujibu wa taarifa za Kiintelijensia, Sheikh Ponda ni mhamasishaji wa watu kwenda kuvamia eneo hilo.
Hata hivyo, alipohojiwa baadaye na Wakili Kweka pamoja na wakili wa upande wa utetezi, alidai mmiliki wa sasa wa eneo hilo ni Suleiman na kwamba, Hafidh alikuwa ni ripota tu aliyetumwa na mmiliki Suleiman.
Pia akihojiwa na Wakili wa upande wa utetezi, Juma Nassoro, Juma alidai hakumbuki nyaraka zinazothibitisha uhalali wa Hafidh kumiliki eneo hilo.
Vilevile, hakujibu swali aliloulizwa na wakili huyo kama kwenye waraka wa maelezo ya Sheikh Ponda aliyoyatoa polisi kuna sehemu inayoonyesha alieleza kuhamasisha watu kwenda kuvamia eneo hilo.
Aidha, Wakili Nassoro alimhoji kama Jeshi la Polisi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wana mamlaka kisheria ya kutatua mgogoro wa ardhi, Juma alijibu kuwa hawana.
Alipoulizwa na wakili huyo nani mwenye mamlaka hayo? Alijibu kuwa ni Mahakama ya Ardhi.
Vilevile, Juma alidai Sheikh Ponda katika maelezo yake aliyoyatoa polisi alisema kama kuna mtu anayesema eneo hilo ni lake aende mahakamani na kwamba, mtu anayedai hivyo, hajaenda mahakamani.
Alidai hoja ya wanaopinga Bakwata na anayedaiwa kuwa ni mmiliki ya kubadilishana eneo hilo na la Kisarawe, inadai kuwa Bakwata haina uwezo wa kufanya mabadilishano hayo.
Hivyo, alidai kati ya Sheikh Ponda na wenzake pamoja na Bakwata kuna hoja zinazokinzana kuhusiana na mabadilishano ya maeneo hayo. Kesi hiyo itaendelea leo.


Post a Comment

Previous Post Next Post